IQNA

Hali ya Waislamu India

India yafunga shule baada ya mwalimu kuwaamuru watoto wamchape vibao mwanafunzi Muislamu

16:42 - August 29, 2023
Habari ID: 3477516
UTTAR PRADESH (IQNA) - India mnamo Jumatatu ilifunga shule katika jimbo la kaskazini mwa India la Uttar Pradesh baada ya mwalimu wake kuwataka wanafunzi kumpiga vibao mwanafunzi mwenzao Mwislamu.

Mwalimu huyo amekamatwa na uchunguzi wa kesi hiyo unaendelea, afisa wa elimu Shubham Shukla alisema katika taarifa yake na kuongeza kuwa utambuzi wa shule hiyo itafutiwa usajili.

Kulikuwa na ghadhabu kubwa baada ya video ya tukio hilo katika kijiji cha Khubbapur huko Muzaffarnagar kusambaa mitandaoni siku ya Ijumaa. Vidio hiyo iliyosambaa, inamuonyesha Trapta Tyagi, mwalimu wa skuli ya Uttar Pradesh, jimbo lenye watu wengi zaidi nchini India, akitoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu pamoja na kuwahimiza wanafunzi wengine wampige makofi makali zaidi mwenzao huyo mwenye umri wa miaka saba.

Katika vidio hiyo, inasikika kwa nyuma sauti ya kiume ikikubaliana na agizo la mwalimu huyo.

"Nimetangaza kwamba watoto wote wa Kiislamu wanapaswa waondoke," Tyagi anasikika akisema kwenye vidio hiyo.

"Uko sahihi, inaharibu elimu," mwanamume huyo anasikika akisema wakati mtoto huyo Muislamu mwathirika akisimama mbele ya darasa huku akiomboleza kwa hofu.

Wazazi wa mtoto huyo Mohammad Altamash, wamevieleza vyombo vya habari kwamba tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi katika Skuli ya Serikali ya Neha katika kijiji cha Kubbapur, kilomita 30 kutoka mji wa Muzaffarnagar.

"Jana, mwanangu alikuja nyumbani akilia," ameeleza Rubina, ambaye ni mama wa mtoto na kuongezea kwa kusema “alipatwa na kiwewe. Hivi sivyo inavyopasa kuwatendea watoto.”

Kulingana na babake Mohammad Irshad, mwalimu aliwataka wanafunzi wampige mtoto wake kwa zamu mmoja baada ya mwingine.

Irshad ameongeza kuwa: “Mwalimu alihalalisha matendo yake kwa kusema mwanangu hakudurusu masomo yake. Mwanangu ni hodari katika masomo yake. Anachukua masomo ya tusheni pia. Tunashindwa kuelewa kwa nini mwalimu alimtendea hivi. Inaonekana mwalimu amejawa na chuki,” ameeleza baba huyo mwenye umri wa miaka 42.

Irshad ambaye ni mkulima, amesema udhalilishaji aliofanyiwa mwanawe ni matokeo ya "chuki ambayo inaenezwa dhidi ya Waislamu nchini India", iliyodhihirishwa na maoni ya mwalimu huyo yaliyosikika kwenye vidio hiyo.

Amesisitiza kuwa, ingawa mwalimu huyo alikubali kosa lake na kuomba msamaha kwa kitendo chake hicho lakini atamhamisha mtoto wake na kumpeleka skuli nyingine. Waislamu ni takribani khumsi (moja ya tano) ya wakazi milioni 235 wa jimbo la Uttar Pradesh. Skuli ulipotokea mkasa huo ina wanafunzi Wahindu na Waislamu.

3484958

Habari zinazohusiana
Kishikizo: india waislamu
captcha