IQNA

Waislamu India

India: Mwanamke Mwislamu alazimishwa kuvua Hijabu wakati wa Mtihani

17:57 - August 22, 2023
Habari ID: 3477480
NEW DelHI (IQNA) – Mwanamke Mwislamu alikabiliwa na ubaguzi katika shule moja huko Tamil Nadu, India, alipotakiwa kuvua hijabu yake wakati wa mtihani.

Shabana, ambaye pia ni mwalimu wa lugha ya Kiarabu, alikuwa amejiandikisha kufanya mtihani wa Kihindi katika Shule ya Upili ya Annamalai Matriculation katika kijiji cha Somasipadi. Aliingia kwenye jumba la mitihani akiwa amevalia Hijabu yake kama kawaida, lakini punde si punde alikabiliwa na msimamizi wa shule hiyo, Revathi, ambaye alimwambia avue Hijabu mara moja.

Revathi alidai kwamba alikuwa akifuata maagizo ya Hindi Prachar Sabha, shirika linalofanya mtihani. Shabana alikataa kutii, akisema kwamba Hijabu yake ilikuwa sehemu ya utambulisho wake wa kidini na chaguo la kibinafsi. Alisisitiza kuwa hakuna sheria inayokataza kuvaa Hijabu wakati wa mitihani.

Hali ilizidi kuwa mabishano makali, na wakuu wa shule wakawaita polisi kuingilia kati. Wanafamilia wa Shabana waliokuwa wakisubiri nje ya ukumbi wa mtihani nao walijiunga na mzozo huo. Waliungwa mkono na mashirika kadhaa ya Kiislamu, kama vile Social Democratic Party of India (SDPI), ambao walilaani kitendo cha shule hiyo kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa kidini na haki za binadamu.

Polisi walijaribu kutuliza pande zote mbili na kutafuta suluhu, lakini Shabana aliamua kutoka nje ya ukumbi wa mtihani bila kumaliza mtihani wake.

Mateso aliyopata Shabana yanaakisi changamoto na mapungufu ambayo wanawake wengi wa Kiislamu wavaao Hijabu wanakumbana nayo nchini India, ambapo mara nyingi wanabaguliwa, kunyanyaswa, na kufanyiwa ukatili kwa sababu ya kuchagua mavazi yao.

3484879

Habari zinazohusiana
Kishikizo: waislamu india
captcha