IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Muamala wa Karne utakufa kabla ya Trump kufa, unaonesha hila na utapeli wa Marekani

18:55 - February 05, 2020
Habari ID: 3472444
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mpango wa Marekani uliopachikwa jina la Muamala wa Karne utakufa hata kabla ya Trump mwenyewe kufa na kuongeza kuwa, njia ya kukabiliana na mpango huo ni kusimama kidete na kufanya jihadi kishujaa taifa na makundi ya Palestina pamoja na uungaji mkono wa ulimwengu wa Kiislamu kwa taifa hilo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumatano asubuhi mjini Tehran alipoonana na maelfu ya wananchi wa Iran wa matabaka tofauti na huku akigusia kitendo cha Marekani cha kuzindua kibeberu na kijuba mpango wake unaoitwa Muamala wa Karne amesema, viongozi wa Marekani wako katika ndoto ya kufanikiwa mpango wao ulio dhidi ya taifa la Palestina baada ya kuupa jina kubwa lakini kitendo chao hicho ni cha kipumbavu na kikhabithi na hapa hapa mwanzo kabisa, tayari mpango huo umeshakuwa kwa madhara yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mpango unaoitwa "Muamala wa Karne" unaonesha wazi hila na utapeli wa Marekani na kufafanua zaidi kwa kusema: Wamarekani wamefanya muamala na Wazayuni kwa kitu ambacho si mali yao.

Ayatullah Khamenei amesema, kitendo cha baadhi chache ya viongozi wasaliti wa nchi za Kiarabu cha kuukubali na kuupigia makofi mpango huo hakisaidii kitu kwani hata katika nchi zao hawana thamani wala itibari. Jambo hilo limekuwa na madhara pia kwa siasa kuu za waistikbari wa dunia wanaopigania muda wote kuisahaulisha kadhia ya Palestina kwani hivi sasa Waislamu na wapenda haki pamoja na makundi yote ya Palestina yameamshwa zaidi na njama hizo na sasa hivi dunia nzima watu wanazungumzia jinsi wananchi wa Palestina wanavyodhulumiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia juhudi za mabeberu za kujaribu kufanikisha mpango huo kwa kutumia vitisho, silaha na fedha na kusisitiza kuwa, tunaamini kwamba taasisi zenye silaha za Palestina zitasimama imara, muqawama utaendelea na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo kwa upande wake itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuyaunga mkono makundi ya Palestina kwani uungaji mkono huo ndilo jambo linalotakiwa na mfumo wa Kiislamu na taifa la Iran.

Vile vile amesema, utatuzi hasa wa kadhia ya Palestina ni njia ya kimsingi iliyopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukubaliwa na jamii ya kimataifa nayo ni kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha Wapalestina wote asili, ili waamue mustakbali wa nchi yao.

Mwisho amesema, Insha'Allah lengo hilo litafikiwa na kwamba nyinyi vijana wa zama hizi mtashuhudia kufikiwa lengo hilo kwa taufiki ya Allah na kwa taufiki Yake Mwenyezi Mungu, mtakwenda kusali ndani ya Baytul Muqaddas.

3876652

captcha