IQNA

Rais wa Afrika Kusini

Mapendekezo ya Trump ya Muamala wa Karne yanafanana na ya mfumo wa 'apatheidi'

17:48 - February 10, 2020
Habari ID: 3472459
TEHRAN (IQNA) - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema mapendekezo ya Rais Donald Trump kwenye 'muamala wa karne' kuhusu Palestina yanashabihiana na mfumo wa kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apatheidi) uliowahi kutawala nchi yake.

Ramaphosa ambaye Jumapili alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika ameuambia umoja huo kuwa, "Nikisikiliza na kusoma yote yaliyosemwa na kuandikwa kuhusu mapendekezo hayo, fikra zangu zinarejea nyuma kwenye kumbukumbu za historia mbaya ambayo wananchi wa Afrika Kusini walipitia katika kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apatheidi) miaka ya 90." 

Amesema mpango huo wa Trump kuhusu Palestina umeibua kumbukumbu za historia mbaya ya Afrika Kusini. "Utawala wa apatheidi uliwahi kuleta mfumo wa Bantustan bila kuwashauri watu wa Afrika Kusini," amesema Ramaphosa. 

Mfumo wa bantustan wa Afrika Kusini ulianzishwa na utawala wa Wazungu waliokuwa wachache ambapo maeneo makubwa yenye rutuba yalitengwa kwa ajili ya Wazungu ilhali Waafrika wazalendo walitakiwa kuwa na maeneo kadhaa tu walipokuwa na haki ya kukaa lakini katika maeneo mengine waliruhusiwa kukaa kama wafanyakazi kwa muda tu.

Naye Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ambaye ni mwenyekiti anayeondoka wa AU amesema katika hotuba yake mbele ya umoja huo kuwa, kadhia ya Palestina itasalia katika nyoyo na fikra za wananchi wa Afrika.

Hapo jana pia, Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema kuwa, mpango wa Muamala wa Karne uko dhidi ya Wapalestina na unakinzana na sheria za kimataifa.

Wazungumzaji wote katika kukao hicho wamegusia pia swala la Palestina na kubaini uungwaji wao mkono kwa madai ya Wapalestina. 

Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel walizindua mpango huo wa kibaguzi walioupa jina la 'Muamala wa Karne' tarehe 28 Januari mwaka huu. Hata hivyo mpango huo umeendelea kupingwa katika kila pembe ya dunia.

3470603

captcha