IQNA

Jinai za Israel

Mkuu wa Haki za Umoja wa Mataifa: Hali katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni janga

17:34 - March 04, 2023
Habari ID: 3476657
TEHRAN (IQNA) - Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu ametoa tahadhari kutokana na wito wa waziri wa utawala wa Israel ambaye ametaka kuangamizwa kwa kijiji kizima cha Wapalestina.

Volker Turk aliyasema hayo siku kadhaa baada ya waziri wa fedha wa utawala haramu wa Israel Bezalel Smotrich kusema kijiji cha Wapalestina cha Huwara "kinahitaji kuangamizwa," na kuongeza kuwa anafikiri "Israel inapaswa kufanya hivyo."

Akizungumza mbele ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Turk alilaani matamshi hayo akisema ni "kauli  kuchochea ghasia na uhasama."

"Hali katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni janga, janga kubwa kwa watu wa Palestina," Turk ameliambia Baraza la Haki za Kibinadamu alipokuwa akiwasilisha rasmi ripoti kuhusu hali katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Waziri huyo wa Israeli alitoa kauli hizo za kutaka Wapalestina waangamizwe kwa umati baada ya mamia ya walowezi Kizayuni waliokuwa na silaha kushambulia kijiji cha Huwara na vijiji vya jirani na kuteketeza makumi ya nyumba na magari.

Mpalestina mmoja aliuawa wakati wa uvamizi wa walowezi na wengine takriban 390 walijeruhiwa, huku vyombo vya habari vya Palestina vikiripoti kuwa Wapalestina walichomwa visu na kushambuliwa kwa vyuma na mawe.

Vikosi vya utawala haramu wa Israel na walowezi wamezidisha vitendo vyao vya kuua na uchokozi dhidi ya Wapalestina tangu mwishoni mwa Disemba 2022, wakati Benjamin Netanyahu aliporejea kama Waziri Mkuu wa utawala huo akiongoza baraza la mawaziri la vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na za Waorthodoksi.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, Wapalestina wasiopungua 68 wameuawa shahidi katika hujuma za wanajeshi katili wa Israel na walowezi wa Kizayuni na miongoni mwa waliouawa kuna idadi kubwa ya watoto.

Turk alionya baraza hilo kwamba "ghasia zinazoongezeka zinawalenga watu wasio na hatia," akitoa wito kwa "wafanya maamuzi...kurudi nyuma kutoka kwenye dimbwi la itikadi kali."

Kwingineko katika matamshi yake, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alitoa wito wa moja kwa moja kwa utawala ghasibu wa Israel kukomesha ukaliaji mabavu maeneo yote ya Wapalestina.

Utawala bandia wa Israel uliundwa mwaka 1948 baada ya kuyakalia kwa mabavu maeneo makubwa ya Wapalestina wakati wa vita vilivyoungwa mkono na madola ya Magharibi.

Israel ilinyakua ardhi nyingi zaidi, yaani Ukingo wa Magharibi, pamoja na al-Quds (Jerusalem) Mashariki, na Ukanda wa Gaza, katika vita vingine vya 1967.

Tangu wakati huo utawala dhalimu wa Israel umejenga mamia ya vitongoji haramu vya walowezi kwenye maeneo yaliyovamiwa na kuweka vikwazo vikali zaidi kwa harakati za Wapalestina huko.

Wakati huo huo, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amelaani matamshi ya kibaguzi na kiichochoze yaliyotolewa na waziri huyo wa fedha wa Israel akitaka kufutwa kabisa kitongoji cha Huwara cha Wapalestina katika uso wa dunia.

Stephane Dujarric amesema kuwa msimamo wa Waziri wa Fedha wa Israel ni wa kichochezi, haukubaliki na unakinzana na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Amesema matamshi ya waziri huyo ni ya kichochezi na si ya kuwajibika hasa kwa kuzingatia kwamba yametolewa na afisa wa serikali. Amesema, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatoa wito wa kujiepusha na matamshi ya chuki na uchochezi. 

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameyataja matamshi ya Smotrich, yanayohimiza kufutwa kikamilifu kitongoji cha Wapalestina cha Huwara huko Nablus, kuwa ni ya kigaidi na kibaguzi.

Mohammad Shtayyeh amesema kwamba matamshi ya Smotrich kwa hakika ni uchochezi rasmi wa kufanya mauaji mapya ya umati dhidi ya raia wa Palestina katika kitongoji cha "Huwara" na makazi na vijiji vingine vya Wapalestina.

Shtayyeh ameutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na mashirika yote ya kimataifa kulaani matamshi hayo na kutekeleza maazimio ya kimataifa kuhusu vikwazo dhidi ya Israel na kuuadhibu utawala huo kwa uhalifu wake dhidi ya raia wa Palestina.

3482692

captcha