IQNA

Jinai za Israel

Utawala katili wa Israel waendeleza jinai Gaza

10:15 - December 02, 2023
Habari ID: 3477972
TEHRAN (IQNA)- Kuanzia jana subuhi Ijuumaa, na mara baada ya kumalizika muda wa kusimamisha vita, utawala wa Kizayuni umeendeleza mauaji ya kikatili kupindukia dhidi ya wananchi wa Ghaza huko Palestina wanaoendelea kuzingirwa kila upande.

Takriban Wapalestina 110 walikuwa wameshauliwa shahidi na mashambulizi ya kinyama ya Israel huko Ghaza. 

Hayo yameripotiwa huku Wizara ya Afya ya Ghaza ikihimiza kufunguliwa kivuko cha Rafah kwa ajili ya kuwafikishia misaada wananchi wa Ukanda huo.

Mwito huo umetolewa baada ya malori ya misaada kukwama tena na kushindwa kuingia Ghaza kutokana na mashambulizi hayo ya kikatili ya ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni. 

Msemaji wa kivuko cha mpakani cha Rafah anasema, malori ya misaada kama mafuta na gesi ya kupikia kutoka Misri kuelekea Ukanda wa Ghaza yamekwama tena kwa sababu utawala wa Kizayuni umeanzisha tena mashambulizi yake dhidi ya wananchi wa ukanda huo.

 

Misaada iliyotolewa na mataifa mbalimbali ambayo inatumia kivuko cha Rafah kuingia Ghaza iliongezeka wakati wa usitishaji vita wa wiki moja, ingawa maafisa wa misaada wanasema bado misaada hiyo ni kidogo sana ikilinganishwa na mahitaji mengi yaliyoko huko Ghaza. 

Kivuko cha Rafah ndiyo njia pekee ya kuingiza misaada ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Ghaza. Tarehe 21 Oktoba, misaada kidogo iliruhusiwa kuingia kwenye ukanda huo baada ya mashambulizi ya takriban siku 50 ya Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ghaza. 

Lakini pia utawala wa Kizayuni haukuwa ukiheshimu ipasavyo makubaliano ya kusimamisha vita ya wiki moja kiasi kwamba, mara kwa mara duru za Palestina zilikuwa zinalaani vitendo vya Israel vya kutoheshimu mapatano hayo.

Marekani imeidhinisha jinai

Wakati huo huo, harakati za Kiislamu au Muqawama  huko Palestina zimejibu jinai mpya za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, wa kubebeshwa dhima na lawama za kuanza tena mapigano ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Usama Hamdan, kiongozi mwandamizi na wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alisema jana jioni kuwa, utawala wa Kizayuni na Marekani ndio wanaopaswa kubebeshwa lawama zote za kuanza upya mashambulizi ya kinyama na kuendelea kuuliwa kidhulma wananchi wa Palestina.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kupita takriban siku 50 za mashambulio ya mfululizo ya jeshi katili la Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza, hatimaye kulianza kutekelezwa makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku nne kwa upatanishi wa Qatar.

Makubaliano hayo yaliongezewa muda kidogo kidogo na kufikia wiki moja huku utawala wa Kizayuni ukilazimika kutii matakwa ya wanamapambano wa Palestina hasa kusimamisha vita, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia kwenye Ukanda wa Ghaza pamoja na mabadilishano ya mateka ambapo utawala wa Kizayuni ulilazimika kukubali masharti ya muqawama wa Palestina ya kubadilisha kila mateka watatu wa Palestina kwa mateka mmoja tu Mzayuni.

/4185109

Habari zinazohusiana
captcha