IQNA

Diplomasia

Rais wa Iran abainisha mafanikio ya safari yake nchini Syria

23:15 - May 05, 2023
Habari ID: 3476962
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea ziara yake ya siku mbili nchini Syria kama hatua ya mabadiliko katika kukuza uhusiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama baina ya nchi mbili na kuongeza kuwa lengo kuu la safari hiyo lilikuwa ni kuenzi muqawama au mapambano ya serikali na taifa la Syria.

Rais Raisi aliyasema hayo katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran mapema Ijumaa aliporejea kutoka safari ya siku mbili nchini Syria. Ameongeza kuwa: "Kwa kuzingatia uungaji mkono wa miaka 12 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa makundi ya muqawama yenye makao yake nchini Syria pamoja na kusimama kidete taifa na serikali ya Syria dhidi ya njama na fitina za maadui, safari ya siku mbili katika nchi hii ya Kiarabu  ina umuhimu mkubwa kwa nchi hizi mbili na kwa eneo zima la Asia Magharibi.”

Rais Raeisi alisema Iran na Syria zina fursa na misingi ya kutosha ya ushirikiano ili kuboresha uhusiano wa kiuchumi, na kuongeza kuwa alizungumzia zaidi masuala ya kifedha na biashara wakati wa mikutano na mwenzake wa Syria Bashar al-Assad.

Ameongeza kuwa, kushirikiana katika uga wa uzalishaji na usambazaji wa umeme, kuanzisha benki ya pamoja na kampuni ya bima, kupunguza ushuru wa biashara kati ya nchi hizo mbili, kupanua njia za usafiri kati ya Iran, Iraq na Syria pamoja na kufufua sekta za kilimo, viwanda na nishati Syria ni kati ya masuala ya msingi yaliyojumuishwa katika hati 14 za ushirikiano zilizotiwa saini kati ya pande hizo mbili.

Taarifa ya mwisho iliyotolewa mwishoni mwa ziara rasmi ya siku mbili ya Raisi nchini Syria, iliyoanza Jumatano na ambayo ilikuwa ya kwanza kwa rais wa Iran katika taifa hilo la Kiarabu katika kipindi cha zaidi ya miaka 13, ilisema kuwa pande hizo mbili zimeeleza kuridhishwa na ushirikiano wa pamoja katika mapambano dhidi ya ugaidi na misimamo mikali. Nchi hizo mbili zimeazimia kuendelea kufanya kazi pamoja hadi kuangamizwa kabisa makundi yote ya kigaidi nchini Syria.

Raisi na Assad pia walifanya mazungumzo ya kina kuhusu njia za kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wa kindugu na wa kimkakati kati ya Tehran na Damascus, na pia walibadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni ya kikanda na kimataifa.

Marais hao wawili walisisitiza haja ya kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja kwa mujibu wa malengo na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Aidha walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande zote kwa kuendeleza maingiliano ya kisiasa, kiuchumi na kibalozi, pamoja na kubadilishana wajumbe wa ngazi za juu kati ya nchi hizo mbili.

Raisi na Assad walishutumu kwa maneno makali mashambulizi ya anga ya utawala haramu wa Israel katika maeneo mbalimbali nchini Syria na kuyataja kuwa ni sababu ya kuleta taharuki katika eneo la Asia Magharibi, na kuashiria haki halali ya Syria kujibu kwa njia inayofaa vitendo hivyo vya uchokozi.

4138622

captcha