IQNA

Harakati ya Hizbullah

Hizbullah daima imekuwa bega kwa bega na watu wanaodhulumiwa

12:29 - August 23, 2022
Habari ID: 3475666
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitizia kwamba harakati hiyo daima imekuwa bega kwa bega na watu wanaodhulumiwa katika eneo la Asia Magharibi wakiwemo wa Yemen, Iraq na Afghanistan.

Sayyid Hassan Nasrallah ameyasema hayo katika hotuba ya ufungaji wa sherehe za kuadhimisha "Machipuo Arubaini" kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 tangu ilipoasisiwa harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya Lebanon ambayo ni maarufu kama Hizbullah na kuongeza kwamba uungaji mkono huo utaendelea pia katika awamu ijayo.

Katika hotuba yake hiyo, Nasrallah ameashiria pia uhusiano imara ambao umekuwepo kati ya Hizbullah na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 40 na akabainisha kuwa Iran imeiunga mkono harakati hiyo na makundi mengine ya Muqawama.

Katibu Mkuu wa Hizbullah alitamatisha hotuba yake kwa kumzungumzia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema: "Ayatullah Khamenei daima amekuwa akiipa umuhimu maalumu Hizbullah, hivyo inapasa tumshukuru, kwani katika muda wa miaka 40 mara zote amekuwa mitihili ya baba mwenye huruma, mweledi na shujaa na hajawahi kutuacha mkono hata chembe".

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon katika sehemu nyingine ya hotuba yake amesema ushindi wa mwaka 2000 wa Muqawama ulihitimisha mradi wa "Israel Kubwa."

Nasrullah ameeleza kuwa kuna mafungamano makubwa baina ya harakati zilizoendeshwa na Muqawama kabla ya mwaka 1982 na baada yake, kwa namna ambayo ushindi wa mwaka 2000 ulitamatisha mradi wa Israel Kubwa na kulisambaratisha jeshi lililokuwa halishindiki.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: wapiganaji wa Hizbullah wanamfuata Imamu Khomeini (MA) na sira yake; na kwao wao, yeye ndiye zaidi aliyeipa ilhamu harakati hiyo katika zama hizi.

Amebainisha pia kuwa, mafanikio ya karibuni zaidi ya muqawama yalikuwa ya mwaka 2006 ambapo uliweza kurejesha haki za mafuta na gesi za Lebanon. Ameongezea kwa kusema: kukomboa ardhi zilizosalia za Lebanon zinazokaliwa kwa mabavu ni jukumu la kitaifa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sayyid Hassan Nasrullah amesema, suala la Palestina ni sehemu ya dini, utamaduni, heshima na utukufu wa taifa hilo, kwa hiyo haileti maana kuwa na mtazamo wa kuachana na suala hilo, kutoegemea upande wowote au kulegeza msimamo juu ya kadhia hiyo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongezea kwa kusema: msingi wa mkakati wetu kuhusu suala la Palestina ni kushikamana na mapinduzi ya watu wa Palestina na kupinga mapatano na uanzishaji uhusiano wa kawaida.

Kuhusiana na Syria, Nasrullah amesema, nchi hiyo ni msingi wa mhimili wa Muqawama, vuguvugu endelevu na upinzani dhidi ya dhana ya kusalimu amri mbele ya masharti ya Israel.

3480193

 

captcha