IQNA

Ubaguzi wa rangi Israel

Wabunge Ufaransa waidhinisha azimio la kulaani ubaguzi wa rangi Israel

22:02 - July 23, 2022
Habari ID: 3475527
TEHRAN (IQNA)- Wabunge katika Bunge la Kitaifa la Ufaransa wametia saini rasimu ya azimio la kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi au apatahidi na jinai za kivita dhidi ya Wapalestina.

Azimio hilo ambalo lina kichwa kisemacho: "Kutaasisishwa Utawa wa Apathaidi Dhidi ya Watu wa Palestina" limeidhinishwa na wabunge 38 wa Bunge la Kitaifa la Ufaransa ambao wanawakilisha mrengo wa kushoto wa NUPES.

Awali rasimu hiyo ilikuwa imewasilishwa Julai 13 na mbunge wa chama cha Kikomunisti Jean-Paul Lecocq na kuibua mjadala mkubwa Ijumaa. Kati ya waliotia saini rasimu hiyo ni mgombea urais wa zamani Fabien Roussel.

Rasimu hiyo imewakasirisha sana Wazayuni na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni barani Ulaya kwani imeitaja Israel kuwa ni ' utawala wa ubaguzi wa rangi au apatahidi'. Hali kadhalika rasimu hiyo imeulaani utawala ghasibu wa Israel kwa kuanzisha mfumo wa ukandamizaji na jinai za kivita dhidi ya Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu.

Mwaka jana mkutano mkuu wa chama cha Leba nchini Uingereza ulipiga kura na kupitisha hoja ya kuitambua Israel kuwa ni utawala unaotenda jinai ya ubaguzi wa Apathaidi, na kukifanya kuwa chama cha kwanza kikubwa cha siasa barani Ulaya kuchukua msimamo huo dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni.

Mwezi Aprili pia shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliitaja Israel kuwa utawala wa kibaguzi na kutangaza kuwa, mauaji na mateso yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina na kuwanyimwa haki zao ni uhalifu na jinai dhidi ya binadamu.

Amnesty International imeandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Ubaguzi wa rangi (apartheid) sio jambo lililopita na la kihistoria tu, bali pia ni ukweli na hakika inayowasumbua kila siku mamilioni ya Wapalestina katika maeneo yao yanayokaliwa kwa mabavu na inaendelea hadi hii leo." 

4072815

captcha