IQNA

UN: Mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Kamanda Soleimani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa

18:05 - February 20, 2020
Habari ID: 3472490
TEHRAN (IQNA) - Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard amesema Marekani ilikiuka sheria za kimataifa kwa kumuua , Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard ametoa ripoti Kuhusiana na mauaji hayo ya kigaidi akisisitiza kuwa, yalikuwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Callamard amesema mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Kamanda Soleimani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na hatua hiyo ya Marekani inaweza kuweka msingi wa mwenendo mbaya ambao hatimaye utakuwa na maafa makubwa. 

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Mauaji ya kigaidi ya Jenerali Qassem Soleimani yamekanyaga kikamilifu vigezo vinavyohusiana na matumizi ya nchi ya nguvu za kijeshi nje ya mipaka yake. Katika tukio hilo afisa wa serikali alishambuliwa ilhali hapo awali watu wasio maafisa wa serikali walikuwa wakishambuliwa; na hatua hii ni ukiukaji mkubwa wa kanuni na sheria za kimataifa."

Tarehe 3 mwezi uliopita wa Januari Rais Donald Trump wa Marekani alikiuka sheria za kimataifa na kutoa amri ya kuuliwa kigaidi aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wenzake kadhaa karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq alikokuwa ameenda safarini kwa mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Kaimu Mkuu wa kikosi cha wapiganaji wa kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hashul Shaabi, Abu Mahdi Al Muhandes wakiwa pamoja na wenzao 8, walishambuliwa na ndege za kivita za askari magaidi wa Marekani alfajiri ya tarehe 3 Januari karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad na kuuliwa shahidi. Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza kuwa, amri ya mauaji hayo ilitolewa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo. Kisingizio kilichotumiwa na Trump kuhalalisha mauaji hayo ni madai kwamba, Kamanda Qassem Soleimani alikuwa safari nchini Iraq kwa shabaha ya kupanga mashambulizi dhidi ya Wamarekani na kambi zao za kijeshi na kwamba shambulizi hilo lilikuwa hatua ya kujihami. Maafisa wa serikali ya Iraq wamepinga vikali madai hayo. Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq, Adil Abdul Mahdi tarehe 5 mwezi huo huo wa Januari alihutubia Bunge la nchi hiyo na kusema kuwa: Kamanda Qassem Soleimani alikuwa safari nchini kwa ajili ya kukabidhi majibu ya serikali ya Iran kwa barua ya Saudi Arabia iliyokuwa imewasilishwa na Baghdad kwa serikali ya Tehran.Matamshi haya ya Waziri Mkuu wa Iraq yaliweka wazi zaidi uongo wa serikali ya Washington kuhusiana na sababu za mauaji hayo.

Sasa na baada ya Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard kuitaja hatua hiyo kuwa ilikiuka sheria na kanuni za kimataifa, hakuna tena shaka kwamba Donald Trump na serikali yake ni wakiukaji wakuu wa sheria za kimataifa na hawasiti kukanyaga sheria hizo kwa ajili ya kutimiza malengo na siasa zao za mabavu.

3879789

captcha