IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Kuna tatizo sugu la chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani

19:49 - November 24, 2023
Habari ID: 3477939
BERLIN (IQNA) – Chuki dhidi ya Uislamu ni tatizo kubwa nchini Ujerumani, na kulishughulikia kunahitaji ushiriki wa makundi makubwa ya jamii, mtaalamu mashuhuri amesema.

Mathias Rohe, ambaye alishiriki kuandika moja ya ripoti za kina zaidi juu ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani, alizungumza na Shirika la Habari Anadolu kuhusu kuongezeka kwa hisia dhidi ya Waislamu nchini humo.

"Utafiti wetu umebaini kuwa Waislamu nchini Ujerumani wanakumbana na ubaguzi wa chuki dhidi ya Uislamu katika maisha yao ya kila siku, kwa mfano katika elimu, katika soko la ajira, wakati wakitafuta nyumba, kwenye vyombo vya habari, na mengine mengi," Rohe alisema.

"Ni tatizo la dharura, na tunapaswa kutambua kuwa hili ni tatizo la jamii kwa ujumla. Tusiwaache Waislamu peke yao na hili. Hili ni tatizo letu sote,” alisisitiza.

Kulingana na utafiti wa wataalam wa kujitegemea, ambao ulichapishwa mnamo Juni, hisia za kupinga Uislamu zimeenea katika sehemu kubwa za wakazi wa Ujerumani. Karibu kila mtu wa pili nchini Ujerumani anakubaliana na kauli dhidi ya Uislamu.

Profesa Rohe kutoka Chuo Kikuu cha Erlangen-Nuremberg anasema wakati mamilioni ya Waislamu wamekuwa wakiishi Ujerumani kwa miaka mingi na kuwa sehemu muhimu ya jamii, dhana potofu na kuhusu Waislamu bado zimeenea.

Alisema Wajerumani wengi bado wana dhana potofu kama vile Waislamu hawawezi kuleta mabadiliko yoyote chanya au maadili yao ni tofauti kabisa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kila mtu wa tatu kutoka nchi ya asili ya Kiislamu anakumbana na ubaguzi nchini Ujerumani, mara chache kwa mwezi. Wanawake wa Kiislamu ambao huvaa hijabu mara nyingi huripoti muamala mabaya zaidi katika maisha ya kila siku.

Rohe alisema jinsi vyombo vya habari vinavyoripoti kuhusu migogoro ya sasa ya kimataifa na taswira yake mbaya ya Uislamu na Waislamu ina taathira kubwa kwa mitazamo ya umma.

Rohe pia alidokeza kwamba tangu kuanza vita vya Israel dhidi ya  Gaza mwezi uliopita, Waislamu nchini Ujerumani wanakabiliwa na chuki na tuhuma jumla kwamba wanaihurumia harakati ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas, ambayo inakabilianana Israel.

Idadi ya watu Ujerumaini ni  milioni 84, ambapo miongoni mwao kuna Waislamu milioni tano na hivyo kuifanya idadi ya Waislamu nchini humo kuwa ya pili kwa ukubwa Ulaya Magharibi baada ya Ufaransa. Kumekuwa na ongezeko la ubaguzi wa rangi na hujuma dhidi ya Waislamu nchini humo katika miaka ya hivi karibuni, zikichochewa na propaganda za vyama na vuguvugu la siasa kali za mrengo wa kulia.

Katika nusu ya kwanza ya 2023, polisi walirekodi uhalifu 258 wa chuki dhidi ya Uislamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwenye misikiti, kesi za madhara ya mwili, na barua za vitisho.

Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Berlin, CLAIM, lilionya kwamba kumekuwa na ongezeko la uhalifu wa chuki dhidi ya  Uislamu tangu vita vya Gaza kuanza.

Kundi hilo liliandika visa 53 vya vitisho dhidi ya Waislamu, ghasia na ubaguzi katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mashambulizi 10 kwenye misikiti.

3486147

Habari zinazohusiana
captcha