IQNA

Diplomasia

Azimio la Baraza la Usalama huku Israel ikiendeleza mauaji ya kimbari Gaza

21:56 - November 17, 2023
Habari ID: 3477904
TEHRAN (IQNA)- Uzembe wa Umoja wa Mataifa na hasa mkwamo katika Baraza la Usalama la umoja huo ambao una jukumu muhimu la kulinda amani na usalama wa kimataifa, kuhusu vita vya Gaza, jinai za kivita na mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, umekosolewa vikali kimataifa.

Baada ya kupita siku 40, Baraza la Usalama limepiga hatua ndogo sana kuelekea kumaliza vita vya Gaza kwa kupitisha azimio dhaifu na lisilo na uzito mkubwa. Jumatano baraza hilo lilipitisha kwa wingi wa kura za wanachama wake azimio lililopendekezwa na Malta la kuanzisha usitishaji mapigano wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kufunguliwa vivuko salama kwa ajili ya kuwezesha shughuli za mashirika ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Gaza.

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura za wajumbe 12 kati ya wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama bila upinzani wowote au kutumika kura ya turufu. Wanachama watatu wa kudumu wa Baraza la Usalama, yaani Marekani, Russia na Uingereza, walijizuia kulipigia kura azimio hilo. Azimio hilo limeungwa mkono na nchi 22 za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na UAE, ambayo ni moja ya wajumbe wasio wa kudumu katika Baraza la Usalama.

Kukubalika

Kupitishwa azimio hilo ni ishara ya kukubalika kwake na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, hasa Russia na Marekani, ambapo kila moja iliwasilisha rasimu yake maalumu kuhusu vita vya Gaza, lakini ikapingwa kupitia kura ya turufu ya upande wa pili. Linda Thomas Greenfield, Balozi na Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, ambaye nchi yake haikupigia kura azimio hilo, aliwalaumu baadhi ya wajumbe wa baraza hilo kwa kukataa kuilaani Hamas na kudai kuwa Hamas ndiyo ilianzisha mgogoro wa sasa.

Katika azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama kuhusu Gaza, pande zote zimeombwa kujiepusha kuzuia misaada na huduma zozote za kibinadamu kuwafikia watu wa Gaza. Azimio hilo pia linataka kuachiliwa huru mara moja na bila masharti mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na makundi mengine ya Wapalestina. Linasisitiza kutekelezwa haraka usitishaji mapigano wa kibinadamu na kuanzishwa njia salama katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kutumwa na kufikishwa huko misaada ya kibinadamu.

Mtazamo wa Russia kuhusu Kusitishwa vita siku chache

Moja ya vipengee vya azimio hilo kinazungumzia suala la kusitishwa vita kwa siku chache tu kwa ajili ya kufikishwa misaada ya kibinadamu na majeruhi kuruhusiwa kuondoka na kutafuta matibabu, suala ambalo bila shaka halisaidii lolote katika utatuzi wa mgogoro wa Gaza. Vasiliy Nebenzia, Balozi na Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amesema katika hotuba yake kwamba: "Kusitishwa mapigano kwa ajili ya kufikishwa misaada ya kibinadamu hakuwezi kuwa mbadala wa usitishaji vita huko Gaza."

Kupitishwa azimio hilo kuna maana ya kuwekwa msingi wa kuhitimisha vita huko Gaza licha ya sisitizo la watawala wa Kizayuni hususan Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu la kuendelea na operesheni za kijeshi huko Gaza kwa lengo la kuharibu kabisa nguvu, zana na suhula za Hamas na makundi mengine ya mapambano ya ukombozi wa Palestina. Wazayuni wanadhani kwamba baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, fursa nzuri imejitokeza kwa ajili ya kuyakandamiza makundi ya muqawama wa Palestina huko Ghaza, na kuwa wanaweza kutumia fursa hiyo kuharibu maeneo mbalimbali ya ukanda huo ikiwa ni pamoja na kuua kwa umati maelfu ya Wapalestina. Ni kwa kuzingatia hilo ndipo azimio hilo lililoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likakosolewa vikali na Tel Aviv. Bret Jonathan, naibu mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa, akizungumzia azimio hilo la Baraza la Usalama, amelitaja kuwa "lisilo na maana wala kuhusiana na ukweli wa mambo" na kudai kudai Israel itaendelea kuzingatia sheria za kimataifa na kupambana na magaidi wa Hamas bila kujali maamuzi ya baraza hilo.

Kauli ya mwakilishi wa Palestina

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, azimio hilo limekosolewa na mwakilishi wa Palestina kutokana na ukweli kwamba halikutaja mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Riyadh Mansour, Balozi na Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mpango wa serikali ya sasa ya "Israel" ni kuendeleza mradi wa kuharibu makazi ya watu wa Palestina na kuwalazimisha kuwa wakimbizi. Azimio la Baraza la Usalama halikukemea mashambulizi ya kiholela ya mabomu huko Gaza wala mauaji ya takriban watoto 5,000 wa Kipalestina. Ulipuaji wa mabomu na uvamizi lazima ukomeshwe sasa na misaada ya kibinadamu iruhusiwe kuingia Ukanda wa Gaza.

3486037

Habari zinazohusiana
captcha