IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Pendekezo la kuundwa 'Muungano wa Jumuiya za Kiraia dhidi ya chuki dhidi ya Uislamu'

18:43 - July 30, 2023
Habari ID: 3477359
TEHRAN (IQNA) – Mwanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu wa Bahrain amependekeza kwamba muungano wa taasisi za kiraia katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu uanzishwe ili kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjiwa heshima matakatifu ya Kiislamu.

Baqer Darwish, mkurugenzi wa Jukwaa la Haki za Binadamu la Bahrain ametoa pendekezo hilo katika hotuba yake kwenye kongamano la mtandaoni lililofanyika ili kujadili kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa mtazamo wa haki za binadamu.

Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani (IQNA) lilifanya mkutano huo kwa njia ya intaneti, uliopewa jina la " anuani ya:  "Kuangazia Kuvunjiwa Heshima Qur'ani Tukufu kwa Mtazamo wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu," siku ya Jumapili.

Mohsen Ghanei, mtaalamu wa Iran katika masuala ya kimataifa, Khalil Hassan, mchambuzi wa Bahrain mwenye makao yake nchini Uswidi, na Sheikh Yusuf Qarut, mwakilishi wa Baraza Kuu la Kiislamu la Shia nchini Uswidi, walikuwa miongoni mwa wazungumzaji wengine katika mkutano huo wa mtandaoni.

Katika hotuba yake, Darwish alielezea kudhalilishwa kwa Qur'ani Tukufu hivi karibuni nchini Uswidi na Denmark kuwa ni jinai mbaya dhidi ya kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Alisema Uswidi inahalalisha kuruhusu vitendo hivyo vya kufuru kwa kusema viko ndani ya mfumo wa uhuru wa kujieleza, ambapo idhini hii inaruhusu tu watu wenye msimamo mkali kueneza chuki ya Uislamu na uchochezi wa kidini.

Hakuna sheria ya kimataifa, zikiwemo zile zinazohusiana na haki za binadamu, zinazohalalisha kuruhusu uhalifu huu kutokea, alisisitiza.

Darwish alisema kwamba vitendo kama vile kuchoma Qur'ani vinadhoofisha uthabiti wa jamii na kwa hivyo, makundi ya kutetea haki na vyombo vya kimataifa, pamoja na nchi za Kiislamu, lazima vichukue msimamo dhidi yao.

Wanapaswa kushinikiza kuwepo kwa waraka katika Umoja wa Mataifa unaopiga marufuku kunajisi mambo matakatifu ya Kiislamu, alisisitiza.

Kuna njia tofauti za kukabiliana na vitendo hivi vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu , kama vile kulaani, kususia nchi zinazoruhusu kutokea, na kufanya maandamano ya amani, alisema mwanaharakati huyo.

Ameongeza kuwa pendekezo moja ni kuunda muungano wa taasisi za kiraia katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu ambazo zitafanya kazi kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjiwa heshima matakatifu ya Kiislamu.

Mkutano huo umekuja wakati wimbi jipya la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani vimeanza nchini Uswidi na Denmark tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Nchi za Nordic zinaruhusu kufuru hizo kutokea chini ya kivuli cha kile kinachoitwa uhuru wa kujieleza licha ya kulaumiwa vikali na mataifa ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu na hata mbele ya azimio la Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mapema mwezi huu.

3484562

Habari zinazohusiana
captcha