IQNA

Katika safari ya Rais Ebrahim Raisi nchini Kenya

Iran na Kenya zimetangaza azma ya kuimarisha uhusiano, hasa wa kibiashara

15:15 - July 12, 2023
Habari ID: 3477268
NAIROBI (IQNA)- Marais William Ruto wa Kenya na Ebrahim Raisi wa Iran wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika sekta mbali mbali. Hayo yamebainika katika hotuba za marais hao leo mjini Nairobi baada ya mazungumzo.

Rais wa Iran aliwasili mjini Nairobi alfajiri ya leo kikiwa ni kituo cha kwanza cha safari yake ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Akizungumza mjini Nairobi, Raisi amesema Iran na Kenya zina uwezo mkubwa wa kuimarisha ushirikiano na kuongeza kuwa, kumewekwa lengo la kuimarisha kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi mara 10 zaidi ya ilivyo sasa.

Katika hotuba hiyo baada ya Kenya na Iran kutiliana saini mapatano matano katika nyanja mbali mbali, Raisi amesema uhusiano wa Iran na Kenya unezidi kuimarika. Aidha amesema, kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran imeweza kusimama kidete kukabiliana na vikwazo na sasa imepiga hatua katika sekta mbali mbali za kisayansi, kiteknolojia na kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran ameshukuru serikali na watu wa Kenya kwa  kumkaribisha na ameelezea matumaini kuwa, uhusiano wa Nairobi na Tehran utazidi kuimarika.

Rais Raisi amesifu sera ya Kenya ya kuweka mazingira rafiki kwa biashara za kigeni. Amesema makampuni zaidi ya Iran yataanzisha shughuli zake nchini Kenya na hivyo kufungua njia yao ya kufikia masoko mengine ya Afrika yenye zaidi ya watu bilioni 1.4.

Kenya inataka uhusiano wa kibiashara na Iran

Kwa upande wake, Rais Ruto amesema Kenya itatumia uhusiano mkubwa ilionao na Iran kupanua biashara.

Ameongeza kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili bado kiko chini lakini kuna uwezekano wa kukua. Ameeleza kuwa Kenya na Iran zitaweka utaratibu utakaowezesha mauzo ya nje ya chai, kahawa na nyama zaidi.

Rais Ruto amesema kwamba Kenya pia itatumia uwezo wa Iran katika teknolojia na uvumbuzi ili kujiimarisha kimaendeleo.

Amedokeza kwamba kuanzishwa kwa Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran mjini Nairobi ni jukwaa mwafaka kwa biashara za Iran na Kenya.

Marais Ruto na Raisi mapema leo walishuhudia kutiwa saini makubaliano mapya katika nyanja za kilimo, mifugo, utamaduni na turathi, habari, TEHAMA, uvuvi, makazi na maendeleo ya miji.
Kabla ya kuhutubia waandishi habari na mazungumzo ya jumbe za pande mbili, marais wa Iran na Kenya walikuwa na kikao cha faragha.

Ndege zisizo na rubani za Iran zazinduliwa Kenya

Ndege zisizo na rubani (drone) zinazozalishwa na makampuni ya teknolojia za kisasa nchini Iran zimezinduliwa katika Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Nairobi kwa madhumuni ya kuuzwa masokoni.

Kwa mujibu wa IRNA, ndege zisizo na rubani za kampuni zinazotumia maarifa za Iran, ambazo zina matumizi mawili ya "kunyunyizia" mashamba ya kilimo na pia "uimarishaji wa mashamba" na kubaini iwapo kuna wadudu waharibifu wa shambani, zimezinduliwa leo Jumatano wakati wa safari ya Rais Ebrahim Rais wa Jamhuri ya Kaiislamu ya Iran mjini Nairobi.

Droni hizo zimezinduliwa wakati Sayyid Ebrahim Raisi,  Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  alipotembelea Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran (IHIT) mjini Nairobi kama sehemu ya safari yake nchini Kenya.

Ndege hiyo isiyo na rubani inayojulikana kama Pelikan 2 imetengenezwa na kampuni ya maarifa ya Iran, ambayo ina uwezo wa kipekee kama vile kuandaliwa kwa ajili ya kazi katika kipindi cha dakika 2, kunyunyizia hekta 2 katika kila oparesheni n.k.

Akiwa katika Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran (IHIT) Rais wa Iran amesema jumba hilo ni moja ya vituo vinavyoongoza katika maendeleo ya uuzaji nje wa bidhaa zinazotokana na teknolojia mpya. 

Katika kituo hicho, zaidi ya kampuni 35 za teknolojia mpya za Iran zinazonesha na kusafirisha bidhaa zao nchini Kenya katika nyanja za dawa, vifaa vya matibabu, kilimo, ujenzi n.k.

Safari ya Rais Ebrahim Raisi nchini Kenya leo inatathminiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mabadilishano ya teknolojia na nchi hii ya Afrika Mashariki. Baada ya safari yake nchini Kenya, Rais Raisi ataekelea Uganda na kisha Zimbabwe.

4154615

Kishikizo: Rais Raisi iran kenya
captcha