Sayyid Ibrahim Raisi Ijumaa ya leo amemtumia ujumbe Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki na Wakristo wote duniani kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS (Yesu) akisema kukumbuka tukio la kuzaliwa mtukufu huyo ni fursa nzuri ya kumuenzi Bibi Maryam AS na kukumbuka sifa za kimaadili na ruwaza njema ya kuwapenda wanadamu na kutoa bishara njema kwa watu wanaokandamizwa na kudhulumiwa za Issa Masih mkabala wa dhulma na ukandamizaji wa watawala madhalimu, na vilevile matumaini ya mustakabali mwema kwa wanadamu.
Kesho Jumamosi Disemba 25, 2021, ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Nabii Issa Masih kwa mujibu wa Wakristo waliowengi.
Issa Masih AS ni mmoja wa Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu ambaye ametajwa kwa heshima na taadhima kubwa sana katika Qur'ani Tukufu.
Katika Aya kadhaa, Qur'ani Tukufu inamtambulisha Issa AS na nafasi yake kama mmoja wa Manabii wakuu waliopewa kitabu na sheria na Mwenyezi Mungu.