IQNA

Waziri Mkuu mteule wa Iraq asissitiza kulinda mamlaka ya kitaifa ya kujitawala

11:10 - April 11, 2020
Habari ID: 3472653
TEHRAN (IQNA) -Waziri Mkuu mpya mteule wa Iraq Mustafa al-Kadhimi amesema, mafanikio ya nchi hiyo katika mahusiano ya kimataifa yatapatikana kwa "kuheshimiana na kushirikiana".

Al-Kadhimi amenukuliwa akisema: "Mamlaka ya kitaifa ya kujitawala ndicho kipaumbele changu cha kwanza."

Waziri Mkuu mteule wa Iraq amesisitiza kuwa, serikali haitaruhusu mtu yeyote yule amtusi raia yeyote wa Iraq kwa kumtuhumu kuwa ana mfungamano na maajinabi.

Aidha ameahidi kuwa baraza la mawaziri atakalounda litakuwa mstari wa mbele kutetea Wairaqi na kupambana na kirusi cha corona kinachosababisha maradhi ya COVID-19.

Kauli hiyo ya Mustafa al-Kadhimi imetolewa kufuatiwa hatua za kutia shaka zilizochukuliwa hivi karibuni na Marekani ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Mapema mwezi huu Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilichukua hatua ya kuingiza nchini Iraq mifumo mipya ya makombora ya ulinzi wa anga ya Patriot bila kuipa taarifa serikali ya nchi hiyo, wakati miito inaendelea kutolewa kuwataka askari wa jeshi la Marekani waondoke nchini humo.

Kufuatia uamuzi wa Adnan al-Zurfi wa kughairi kuunda serikali mpya, na kutokana na maafikiano yaliyofikiwa kati ya makundi ya kisiasa ya kuunga mkono kuteuliwa Mustafa al-Kadhimi kuwa waziri mkuu mpya, siku ya Alkhamisi ya tarehe 9 Aprili Rais Barham Salih wa Iraq alimkabidhi rasmi al-Kadhimi jukumu la kuunda serikali mpya.

3890530

captcha