IQNA

Mhusika mkuu wa hujuma za kigaidi Paris auawa

8:58 - November 21, 2015
Habari ID: 3454889
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka nchini Ufaransa imethibitisha kuwa gaidi aliyepanga na kuratibu mashambulizi ya kigaidi ya Paris ameuawa.

Taarifa ya ofisi hiyo imebainisha kwamba, AbdulHamid Abaaoud, raia wa Ubelgiji ameuawa katika operesheni kali ya polisi katika kitongoji cha Saint Denis. Eneo la kaskazini mwa mji wa Paris jana asubuhi lilishuhudia operesheni maalumu ya jeshi la polisi na maafisa usalama wa Ufaransa dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika katika mashambulizi ya siku ya Ijumaa. Hujuma hiyo ya kigaidi iliyofanywa na kundi la kitakfiri la Daesh ilipelekea zaidi ya watu 130 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mji mkuu Paris. Wapelelezi wanasema kuwa mashambulizi hayo yalipangwa nchini Syria na kukamilishiwa nchini Ubelgiji kabla ya kutekelezwa nchini Ufaransa.

Wakati huo huo Kufuatia mashambulizi ya kigaidi nchini Ufaransa wiki iliyopita, chuki, vitisho na hujuma dhidi ya Waislamu na matukufu yao vimeongezeka nchini Marekani.
Viongozi wa Kiislamu nchini humo wanasema hujuma dhidi ya misikiti na maudhi dhidi ya Waislamu vimeongezeka mno ndani ya wiki moja iliyopita hususan katika majimbo ya Florida, Nebraska, Kentucky, Ohayo, Virginia na New York. Ibrahim Hooper, msemaji wa Baraza la Masuala ya Waislamu nchini Marekani anasema kuwa, mustakabali wa Waislamu nchini humo ni wa kutamausha na wenye giza na kwamba Waislamu wawe tayari kukumbana na adha, hujuma na chuki za kuchupa mipaka kutoka kwa Wakristo wenye misimamo mikali.

3454650

captcha