IQNA

Matamshi ya Obama kuhusu Uislamu

10:23 - February 21, 2015
Habari ID: 2876869
Rais Barack Obama wa Marekani amesema kuwa, nchi hiyo haina vita na Uislamu, bali inapambana na watu wanaoupotosha Uislamu.

Akizungumza hivi karibuni kwenye kikao cha siku tatu cha kujadili njia za kukabiliana na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka na kinachohudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 60 duniani mjini Washington, Rais Obama ameongeza kuwa, watu wanaopambana kwa kushirikiana bega kwa bega na makundi kama vile Daesh, ni magaidi na ulimwengu unapaswa kupambana kijeshi na makundi kama hayo. Rais wa Marekani ameongeza kuwa, kulifungamanisha kundi la al Qaeda au Daesh na dini ya Kiislamu, ni sawa na kukubaliana na fikra na mahubiri ya makundi hayo, jambo ambalo si sahihi kabisa. Hii si mara ya kwanza kwa Rais Obama kutoa matamshi ya kirafiki yanayohusiana na Uislamu. Mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2009, Obama alitoa hotuba mjini Cairo, Misri na hata mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo

alisisitizia umuhimu na nafasi ya dini ya Kiislamu ulimwenguni na kuwanyooshea Waislamu mkono wa urafiki. Hii ni katika hali ambayo, sera rasmi za serikali ya Marekani kuhusiana na kadhia ya ulimwengu wa Kiislamu zinakinzana na misimamo ya Rais wake aliyezaliwa akiwa Muislamu. Matatizo ya Marekani na ulimwengu wa Kiislamu ni ya muda mrefu na hata kabla Barack Hussein Obama hajaingia madarakani kwenye Ikulu ya Marekani. Mara baada ya kusambaratika Shirikisho la Kisioveti la Urusi ya zamani katika muongo wa 1990, stratijia za Marekani zilielekezwa zaidi upande wa makundi ya Kiislamu yenye misimamo mikali. Katika kipindi hicho, Marekani ilikuwa na mahusiano na mashirikiano ya karibu na makundi yenye kuchupa mipaka katika ulimwengu wa Kiislamu, na kuandaa mazingira ya kuundwa makundi kama vile al Qaeda na Taleban. Awali makundi hayo yalikuwa yakihudumia maslahi ya Marekani na madola ya Magharibi, lakini baada ya kupita muda na kujipapatua kutoka kwenye udhibiti wa Wamagharibi, hatua kwa hatua makundi hayo yakaanza kuharibu sura na taswira halisi ya dini ya Kiislamu duniani. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, harakati za magaidi wanaodai kuulinda na kuutetea Uislamu zimetatiza na kuhatarisha maisha ya Waislamu duniani. Nchi za Kiislamu kama vile Afghanistan, Iraq, Pakistan, Syria, Yemen, Somalia na Libya zilishuhudia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na waitifaki wake na kusababisha mamia ya maelfu ya Waislamu wa nchi hizo kuuawa.

Shambulio la Septemba 11, 2001 nchini Marekani lilichukuliwa kama kisingizio tosha cha kushadidishwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na fikra za kutaka Uislamu uhofiwe na kuchukiwa katika ulimwengu wa Magharibi. Hii ni katika hali ambayo, Marekani na washirika wake wa Ulaya na wa Ulimwengu wa Kiarabu walipanga njama za kuuangusha utawala wa Syria, kwa kulitumia kundi la kigaidi la Daesh ambalo linahesabiwa kuwa moja kati ya makundi yaliyomwaga damu nyingi na kufanya mauaji ya kutisha katika zama hizi, suala ambalo limeleta maafa na taathira mbaya kwa Uislamu na Waislamu duniani. Hivi sasa baada ya kupita miaka kadhaa ya propaganda chafu za Wamagharibi dhidi ya Waislamu, Ulimwengu wa Kiislamu na wa Kikristo pia umekuwa ukikabiliwa na vitisho vya makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka na magaidi. Hakuna shaka kuwa, matamshi yanayotolewa na viongozi wa nchi kadhaa kwenye makongamano na mikutano ya kimataifa, hayawezi kuunusuru ulimwengu na hatari za makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka. Kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu, kukomeshwa uingiliaji kati, kukatwa uungaji mkono wa tawala za vibaraka na kuheshimiwa matukufu ya Kiislamu ni sehemu tu ya matakwa ya Waislamu ulimwenguni. Iwapo mambo hayo hayatatekelezwa na kuheshimiwa kikamilifu, Waislamu ulimwenguni hawataweza kushawishika kuamini yale yanayosemwa na Obama, kwamba Marekani haina vita na uadui na ulimwengu wa Kiislamu.../mh

2872589

captcha