IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Iran yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi wakati wa Idul Adh'ha

14:54 - June 30, 2023
Habari ID: 3477216
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani jinai ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden au Uswidi na kusema kuwa, kinachotarajiwa kwa serikali ya nchi hiyo ni kuzuia jinai kama hizo na kwamba serikali ya nchi hiyo ndiyo inayobeba jukumu na dhima yote a kuvunjiwa heshima mara kwa mara matukufu ya Kiislamu nchini humo.

Serikali ya Sweden ilitoa kibali kwa raia mmoja wa nchi hiyo kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu wakati wa sikukuu ya Idul Adh'ha na imetetea kitendo chake hicho cha kijinai.

 Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Alkhamisi kwamba kitendo cha serikali ya Sweden cha kutoa kibali rasmi cha kuvunjiwa heshima mara kwa mara matukufu ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu kinaandaa mazingira ya kuvunjiwa heshima matukufu mengine yote ya umma wa Kiislamu na kutojali hisia za mabilioni ya Waislamu duniani tena wakati huu ambapo mamilioni ya Waislamu wamekusanyika katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina kutekeleza ibada tukufu ya Hija.

Aidha ameashiria juhudi za jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binamu za kupigania kuheshimiwa matukufu ya dini tofauti na kusema kuwa, kuvunjia heshima vitabu vitukufu ni dhihirisho la wazi la kuchochea machafuko na kueneza chuki  na uadui, mambo ambayo yanapingana kikamilifu na asili ya kadhia nzima ya haki za binadamu.

Ameongeza kuwa, serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kama walivyo Waislamu wengine na wapigania haki na uadilifu duniani, hawakubaliani hata chembe na utovu wa adabu unaofanywa dhidi ya matukufu ya Kiislamu na wanaitaka serikali ya Sweden kuzuia vitendo viovu kama hivyo na kwamba serikali hiyo ndiyo inayobeba dhima ya uvunjaji wote wa haki za binadamu na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu nchini humo. 

4151219

Kishikizo: uswidi sweden
captcha