IQNA

Maandamano kulaani kushambuliwa msikiti Sweden

20:05 - December 27, 2014
Habari ID: 2637292
Mamia ya Waislamu nchini Sweden waliandamana Ijumaa kulaani kitendo cha kushambuliwa msikiti mmoja kwa bomu la petroli siku ya Alkhamisi.

Shambulizi hilo dhidi ya msikiti mjini Eskilstuna lilisababisha watu 40 kujeruhiwa. Waandamanaji waliokusanyika kwenye msikiti huo ulioharibiwa kidogo na bomu hilo wameitaka polisi kuharakisha uchunguzi na kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria. Msemaji wa polisi nchini Sweden amewaambia Waislamu kuwa maafisa wa usalama wanafanya juu chini kuwatia mbaroni waliofanya hujuma hiyo.

Msemaji wa polisi ya mji huo Lars Franzell, amesema mtu au watu wasiojulikana walirusha bomu la moto katika msikiti huo .
Watu waliojeruhiwa walikimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu na polisi ya Sweden imeanzisha uchunguzi wa shambulizi hilo.
Shambulizi hilo lililolenga msikiti wa mji wa Eskilstuna ulioko umbali wa kilomita 90 kutoka Stockholm limefanyika baada ya kushadidi harakati za kundi la mrengo wa kulia linalopinga Waislamu na kupamba moto mjadala wa kisiasa nchini Sweden kuhusu suala la wahamiaji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu wa Sweden Umar Mustafa anasema mashambulizi dhidi ya Waislamu yameshadidi nchini humo.

Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vimeendelea kukithiri katika miaka ya hivi karibuni barani Ulaya hususan baada ya kupata nguvu vyama vya kisiasa vyenye mielekeo ya kupinga Uislamu, jambo linalotajwa na weledi wa mambo kuwa ni kengele ya hatari kwa mustakabali wa bara hilo.
Kwenye uchaguzi wa mwezi Septemba, chama cha mrengo wa kulia cha Democrat kinachohesabiwa kuwa na misimamo ya kufurutu ada dhidi ya wahajiri na Waislamu kilipata asilimia 13 ya viti katika bunge la Sweden na hivyo kuongeza wasiwasi wa kuzidi chuki dhidi ya jamii ya Waislamu nchini humo.../mh

2634892

captcha