IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Kadhia ya Palestina inaweza kutatuliwa kupitia mapambano, demokrasia

17:28 - February 18, 2020
Habari ID: 3472483
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kusimama kidete katika njia ya muqawama au mapambano na njia ya demokrasia ya kuitishwa kura ya maamuzi ili Wapalestina wenyewe waamue mustakabali wao ndilo suluhisho la kadhia ya Palestina.

Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, mpango wa Marekani uliopewa jina la Muamala wa Karne katu hauwezi kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Dakta Zarif amesema hayo katika mahojiano na tovuti ya Khamenei.ir na kuongeza kuwa, makundi yote ya kisiasa na kijamii ya Palestina kwa sauti moja yanapinga mpango huo wa Kimarekani na Kizayuni.

Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuyasaidia mataifa yanayodhulimiwa katika eneo hili la Asia Magharibi. Dakta Zarif amefafanua kwa kusema, "Iran itaendelea kushirikiana na makundi ya muqawama huko Palestina na katika nchi nyingine za Kiislamu kama vile Lebanon na Syria, mataifa ambayo ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel."

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa kimya cha baadhi ya nchi za Kiarabu mkabala wa dhulma na ukandamizaji wanaofanyiwa Wapalestina na kusisitiza kuwa, baadhi ya madola hayo vibaraka si tu yamefumbia macho kadhia ya Palestina, lakini yameenda mbali zaidi na kuimarisha uhusiano wao na Wazayuni.

Ameongeza kuwa, "baadhi ya madola hayo ya Kiarabu hayana imani na majirani zao katika eneo na hivyo yameamua kununua usalama wao kutoka Marekani na Israel, madola hayo yanananua silaha na zana za kijeshi kutoka tawala hizo za kiistikbari." Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuhusu umoja wa makundi yote ya Palestina na kusema umoja huo unaweza kuwa na nafasi muhimu sana katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

3470674

captcha