IQNA

Sayyed Hassan Nasrallah

Iran ni imara na inastawi licha ya vikwazo, mapambano dhidi ya Marekani yaendelee

17:29 - February 17, 2020
Habari ID: 3472479
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa Marekani ni muhusika wa vita vyote eneo la Asia Magharibi na amesisitiza kuwa, ni lazima kuendesha muqawama katika pande zote kukabiliana na utawala huo wa kibeberu wa Marekani.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo jana katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kutimia siku 40 tangu alipouawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq sambamba na kumbukumbu za mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Amesema kuwa wiki chache zilizopita sambamba na kuwaua shahidi Luteni Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis, serikali ya Marekani ilifanya jinai nyingine ya kuzindua mpango wa Muamala wa Karne. Amezidi kufafanua kuwa msingi mkuu wa harakati ya kukabiliana na mpango huo, ulikuwa msimamo wa pamoja wa Wapalestina na kwamba, Marekani ni dhihirisho la shetani mkubwa, muungaji mkono wa ugaidi na chimbuko la ubeberu duniani na kwa msingi huo ni lazima kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo. 

Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amefafanua kuwa, kwa kuzindua mpango wa Muamala wa Karne, serikali ya Washington imeanzisha vita ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel) na kwamba huo ndio wadhifa wa muqawama, ameongeza kuwa taifa la Palestina na Waislamu wote wanapaswa kupambana na mpango huo kwa kutumia nyenzo za kila namna. Sambamba na kuashiria mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa kwa kusimama imara wananchi mapinduzi ya Iran yameendelea kusonga mbele kila uchao licha ya matatizo na vikwazo mbalimbali dhidi yake. Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameelezea kumbukumbu za mwamko wa wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa na kusema kuwa, watawala wa Bahrain wameigeuza nchi hiyo kuwa kambi ya maridhiano na utawala haramu wa Kizayuni na eneo la kutekeleza njama chafu dhidi ya matukufu ya taifa la Palestina linalodhulumiwa. 

3879221

captcha