IQNA

Mwanajeshi gaidi Thailand awapiga risasi na kuwaua watu 26

19:12 - February 09, 2020
Habari ID: 3472454
TEHRAN (IQNA) - Watu 26 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa nchini Thailand baada ya kupigwa risasi kiholela na mwanajeshi mmoja wa nchi hiyo katika mji wa Nakhon Ratchasima.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Thailand ameziambia duru za habari kwamba, Jakraphanath Thomma, afisa wa madaraka ya chini alimshambulia mkuu wake kabla ya kuiba bunduki na risasi kutoka katika kambi ya kijeshi.

Baadaye mwanajeshi huyo gaidi aliwafyatulia risasi waumini waliokuwa katika hekalu na duka la jumla katika mji huo.

Picha za vyombo vya habari zilionekana zikionyesha mshukiwa huyo akitoka katika gari moja katika eneo moja la duka hilo la jumla katika wilya ya Muang na kuwafyatulia watu risasi kiholela.

Picha nyengine zilionyesha moto nje ya jengo hilo, huku kukiwa na ripoti kwamba ulisababishwa na gesi iliolipuka baada ya kupigwa risasi .

"Mwanajeshi huyo alitumia bunduki ya rashasha kuwapiga risasi watu wasio na hatia na kuwajeruhi wengi huku wengine wakifariki''.

Maafisa nchini Thailand wamesema mwanajeshi huyo alikuwa amekasirishwa na mpango wa ardhi uliokwenda kombo. Waziri Mkuu Prayuth Chan-ocha amewaambia waandishi habari kuwa mwanajeshi huyo alikuwa na mgogoro binafsi juu ya mpango wa nyumba kati ya mwanajeshi huyo na jamaa yake.

Wanajeshi wa Thailand walimpiga risasi na kumuua mwanajeshi huyo baada ya makabiliano ya muda mrefu katika jengo hilo lililoko mjini Nakhon Ratchasima, ambapo ndipo wengi wa wahanga wa mkasa huo walipouliwa.

3877415

captcha