IQNA

Kumbukumbu ya kubomolewa makaburi ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW ya Jannatul Baqii mjini Madina

10:49 - June 13, 2019
Habari ID: 3471999
TEHRAN (IQNA) Jumatano tarehe nane Shawwal 1440 Hijria, sawa na tarehe pili Juni 2019 ni kumbukumbu ya Mawahhabi kubomoa makaburi ya Ahul Bayt wa Mtume SAW ya Jannatul Baqii katika mji mtakatifu wa Madina takribani miaka 97 iliyopita.

Katika tukio hilo la kusikitisha, Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul Bait wa Mtume SAW ambayo yako Baqii, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya Muhammad Ibn Saud kutawala tena maeneo ya Hijaz, likiwemo eneo la Madina, Sheikh Abdullah bin Balihad mmoja wa makadhi wa Mawahabi, alitoa fatwa ya kuhalalisha kuharibiwa kwa makaburi matukufu na ya kihistoria ya mjini Madina. Mawahabi walikusanya watu kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda katika makaburi hayo ya Baqii na kuanza kubomoa na kuharibu kila kitu kilichokuwa juu ya makaburi ya mji wa Madina na nje ya mji huo.

Miongoni mwa makaburi yaliyobomolewa na kuharibiwa vibaya ni makaburi manne ya maimamu na wajukuu wa mtukufu Mtume SAW, makaburi ya Abdullah na Aaminah, wazazi wa tukufu wa Mtume SAW, kaburi la Ibrahim mtoto wa kiume wa Mtume SAW na kaburi la Ummul Banin mama wa Abul Fadhlil-Abbasi. Kaburi pekee lililobakishwa na Mawahabi hao wenye mioyo ya kikatili ni la mtukufu Mtume Muhammad SAW, kwani walijua kuwa kubomoa kaburi la mtukufu huyo kungezua hasira kali ya Waislamu duniani.

Kutokana na taasubi hizo, hadi sasa kumesalia athari chache mno ukilinganisha na zile zilizokwisha haribiwa. Mfano wa wazi wa suala hilo ni makaburi ya Baqii ambayo yanafananishwa na kitabu kikubwa kinachoelezea historia ya Waislamu wa awali. Naam! Baqii sio eneo la makaburi tu, bali ni turathi ya thamani ya dini tukufu ya Kiislamu.

Baada ya Mawahabi kulikalia eneo la Hijaz na kulipachika jina la Saudi Arabia walichukua hatua kinyume na rai za maulama wa Kiislamu ikiwemo kuyavunja makaburi ya watukufu hao. Kubomoa makaburi ya baqii haikuwa jinai pekee iliyotekelezwa na jamii ya watu hao wenye fikra potofu, bali Mawahabi hao waliharibu pia katika maeneo tofauti ya ardhi hiyo ya Hijaz athari muhimu zinazohusiana na Mtume Muhammad SAW, Ahlul-bayt na masahaba zake na uharibifu huo hungali unaendelea leo chini kwa chini kote Hijaz. Mbali na hayo watu wenye fikra za Uwahhabi kote duniani hasa magaidi wakufurishaji kama wale wa ISIS au Daesh, Al Qaeda, Boko Haram na Al Shabab wamekuwa wakimbomoa turathi za Kiislamu huko, Iraq, Syria, Afghanistan, Afrika Magharibi hasa Mali na pia nchini Somalia. Siku chache zilizopita, magaidi wa Kiwahhabi wa ISIS walipozingirwa baada ya kushindwa katika mji wa Mosul Iraq, walilipua kwa mabomu msikiti wa al-Nuri mjini humo ambao ulikuwa na mnara uliojengwa miaka 1000 iliyopita!

Mawahabi ambao ni kundi lenye fikra potofu na mgando, wanajiona kuwa wao ndio Waislamu pekee huku wakiwaita Waislamu wengine katika Mashia na Masuni kuwa makafiri. Wafuasi wa kundi hilo kwa kutumia itikadi batili inayopingana na itikadi sahihi ya tauhidi iliyokuwa ikifuatwa na Waislamu wa mwanzo wa mjini Makka na Madina, walizishambulia vibaya athari za Kiislamu yakiwemo makaburi ya Ahlul Bayt wa Mtume; na kama hiyo haitoshi, watu hao wakapora pia vitu vya thamani vilivyokuwa katika eneo hilo. Tukio hilo lilitokea tarehe 8 Shawaal mwaka 1344 Hijiria sawa na mwaka 1926 Miladia na ulimwengu  unakumbuka tuko hilo kwa majonzi makubwa. Kwa mnasaba wa siku hii Waislamu huandamana kote duniani kubainisha malalmiko yao kutokana na uovu huo wa Mawahhabi huki wakitaka maziara hayo ya waja wema wa Mwneyezi Mungu yajengwe upwa kwani ni sehemu muhimu ya turathi ya Uislamu. 

3818767

captcha